WASHINGTON D.C.–

Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kusitisha kwa muda operesheni ya kijeshi iliyokuwa imepangwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika chapisho lake mtandaoni Truth Social, Rais Trump amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kupokea wito maalum kutoka kwa viongozi wa mataifa ya Ghuba. Viongozi waliohusika katika mazungumzo hayo ni pamoja na Emir wa Qatar, Tamim bin Hamad Al Thani; mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman Al Saud; na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mohamed bin Zayed Al Nahyan.

Rais Trump ameeleza kuwa viongozi hao wamemshawishi kusitisha mashambulizi hayo ili kuruhusu mazungumzo ya kidiplomasia ya ngazi ya juu yaliyopo sasa kuchukua mkondo wake.

“Kufuatia heshima yangu kwa viongozi hao wakuu na washirika wetu, nimewaelekeza Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, na Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Pamoja, Jenerali Daniel Caine, kutotekeleza shambulio lililokuwa limepangwa dhidi ya Iran,” ilisema taarifa hiyo ya Rais.

Rais amesisitiza kuwa lengo kuu la mazungumzo hayo ni kuhakikisha kunapatikana makubaliano yanayokubalika na Marekani pamoja na washirika wake katika Mashariki ya Kati na kwingineko, huku akisisitiza kipaumbele cha kimkakati: “Hatutakubali Iran kumiliki silaha za nyuklia.”

Licha ya kusitisha mashambulizi hayo, Rais Trump ametoa onyo kali kwa Iran. Amesema amewapa maagizo maalum maafisa wake wa usalama na jeshi kuwa katika utayari wa hali ya juu.”Nimeelekeza jeshi la Marekani kuwa tayari kuendelea na shambulio kubwa na la kina dhidi ya Iran wakati wowote, iwapo makubaliano yanayokubalika hayatofikiwa,” aliongeza Rais Trump.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *