Wizara ya Sheria ya Marekani inaripotiwa kuandaa hatua ya kuondoa mashtaka ya udanganyifu dhidi ya bilionea wa India, Gautam Adani, hatua ambayo inaweza kuhitimisha rasmi kesi ya jinai iliyofunguliwa wakati wa utawala wa Rais Joe Biden.
Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la New York Times (NYT), Adani alikuwa akikabiliwa na tuhuma za rushwa na udanganyifu uliodaiwa kuwaathiri wawekezaji wa Marekani.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mabadiliko hayo yamechangiwa na juhudi za timu mpya ya mawakili wa Adani inayoongozwa na Robert J. Giuffra Jr., ambaye ni mmoja wa mawakili binafsi wa Rais wa zamani Donald Trump.
Inadaiwa kuwa mwezi uliopita Giuffra alifanya mazungumzo na maafisa wa Wizara ya Sheria ya Marekani, akisisitiza kuwa upande wa mashtaka haukuwa na ushahidi wa kutosha wala mamlaka ya kisheria kuendesha kesi hiyo.
Katika mazungumzo hayo, timu ya Adani pia ilieleza kuwa mfanyabiashara huyo yuko tayari kuwekeza dola bilioni 10 katika uchumi wa Marekani pamoja na kuunda ajira zipatazo 15,000 iwapo mashtaka dhidi yake yatafutwa.
Hata hivyo, waendesha mashtaka walisisitiza kuwa pendekezo hilo halitakuwa na ushawishi katika uamuzi wa kesi hiyo, ingawa taarifa zinaonyesha kuwa lilipokelewa kwa mtazamo chanya na baadhi ya maafisa waandamizi wa Wizara ya Sheria waliohudhuria kikao hicho.