Gazeti la Wall Street Journal limeripoti kuwa Iran inaendelea kupata nguvu katika vita vya taarifa kupitia uzalishaji na usambazaji wa video kadhaa zilizotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya akili bandia (AI).
Kwa mujibu wa gazeti hilo, video hizo zimeenea kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na zimekuwa sehemu ya mkakati wa kuongeza ushawishi katika majukwaa ya kimataifa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa lengo kuu la video hizo ni kuchochea mgawanyiko wa kisiasa ndani ya Marekani. Imebainishwa kuwa klipu hizo hutayarishwa na kusambazwa na makundi yanayoiunga mkono Iran pamoja na baadhi ya ofisi za kidiplomasia za nchi hiyo.
Mara nyingi video hizo huonesha kwa kejeli hatua na mikakati ya kijeshi ya Marekani. Katika moja ya video zilizotajwa kwenye ripoti, rais wa Marekani, Donald Trump, ameonyeshwa kwa sura ya mharamia katika mandhari yanayofanana na filamu Pirates of the Caribbean.
Video hiyo inaonyesha majeshi ya Marekani yakijaribu kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz na kuizingira bandari za Iran, lakini juhudi hizo zikimalizika kwa kushindwa huku meli za Marekani zikiharibiwa.