Klabu ya Real Madrid imekumbwa na taarifa za sintofahamu baada ya ripoti kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa kudai kuwa viungo wa timu hiyo, Federico Valverde na Aurélien Tchouaméni, walihusika kwenye ugomvi mkubwa uliotokea katika uwanja wa mazoezi wa Valdebebas.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mvutano kati ya wachezaji hao ulianza kabla ya mazoezi kufanyika na baadaye kuendelea hadi ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mazoezi kumalizika.
Ripoti zinaeleza kuwa hali ilikuwa mbaya kiasi cha baadhi ya wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi kulazimika kuingilia kati ili kuwatenganisha wawili hao.
Vyombo vya habari vya Ulaya vimeripoti kuwa Federico Valverde alipata jeraha eneo la kichwa katika tukio hilo na baadaye kupelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi. Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hali yake si mbaya sana.
Chanzo cha mgogoro huo bado hakijawekwa wazi rasmi, lakini baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa kulikuwa na hali ya mvutano ndani ya kikosi hicho kufuatia matokeo yasiyoridhisha ya timu katika kipindi cha hivi karibuni.
Real Madrid imekuwa chini ya presha baada ya kutolewa kwenye michuano ya UEFA Champions League pamoja na kupoteza nafasi muhimu katika mbio za ubingwa wa La Liga dhidi ya wapinzani wao FC Barcelona.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa viongozi wa juu wa Real Madrid waliinisha kikao cha dharura kujadili tukio hilo huku uchunguzi wa ndani ukiendelea kubaini chanzo halisi cha mgogoro huo pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Mpaka sasa, Real Madrid haijatoa tamko rasmi lenye kuthibitisha kwa undani tukio hilo, jambo ambalo limeendelea kuongeza mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka duniani.
Iwapo taarifa hizi zitathibitishwa rasmi, tukio hilo linaweza kuwa miongoni mwa migogoro mikubwa kuwahi kutokea ndani ya kikosi cha Real Madrid katika miaka ya karibuni.