Kyiv — Serikali ya Ukraine imemwita balozi wa Israel nchini humo kutoa malalamiko rasmi kuhusu usafirishaji wa nafaka ambayo Ukraine inadai iliibwa kutoka maeneo ya nchi hiyo yaliyo chini ya udhibiti wa Urusi na kuingizwa katika bandari ya Haifa nchini Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andriy Sybiha, alimwita balozi wa Israel, Michael Brodsky, tarehe 28 na 29 Aprili 2026 na kumkabidhi malalamishi rasmi ya kupinga tukio hilo. Kwa mujibu wa Ukraine, Israel haikuchukua hatua kuhusu mzigo wa awali wa nafaka, huku meli nyingine iitwayo Panormitis ikiripotiwa kusubiri kuruhusiwa kutia nanga.
Ukraine ilisema ilikuwa tayari imeionya Israel mapema mwezi Aprili kuhusu uwezekano wa kuwasili kwa mizigo kama hiyo ya nafaka. Ripoti zinaonyesha kuwa huu ni angalau mzigo wa nne wa aina hiyo kuingizwa nchini Israel tangu mwanzo wa mwaka huu.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Sa’ar, amekanusha madai hayo. Amesema Ukraine haijawasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa nafaka hiyo iliibwa, na kuishutumu Kyiv kwa kutumia vyombo vya habari katika diplomasia yake.
Israel imesisitiza kuwa shughuli hizo ni biashara halali.Wakati huo huo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameonya kuwa nchi zitakazohusika kusafirisha au kufaidika na nafaka hiyo zinaweza kukumbwa na vikwazo. Zelenskyy amesema suala hilo linakiuka sheria za Israel na kwamba Ukraine itashirikiana na washirika wake wa Ulaya kushughulikia tatizo hilo.Mvutano huu unakuja wakati Urusi ikiendelea kudhibiti takribani asilimia 20 ya eneo la Ukraine tangu kuanza kwa vita mwaka 2022. Serikali ya Kyiv tayari imewawekea vikwazo watu na makampuni yanayoshirikiana na mamlaka za Urusi katika maeneo yaliyochukuliwa.