Washington – Rais wa Marekani, Donald Trump, anafahamu kikamilifu athari za kisiasa ambazo vita vimeleta kwake na kwa chama chake, kwa mujibu wa vyanzo vitatu vinavyofahamu mashauriano ya hivi karibuni yaliyofanyika katika Ikulu ya Marekani.
Vyanzo hivyo vimeiambia Reuters kuwa licha ya kuwepo kwa shinikizo kubwa la ndani linalotaka vita vikomeshwe, chaguo za kijeshi bado hazijaondolewa mezani. Hata hivyo, wanasema kuwa mipango mikubwa ya kijeshi, ikiwemo uwezekano wa uvamizi wa ardhini ndani ya Iran, imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wiki zilizopita.
Kwa mujibu wa taarifa za Reuters, ripoti kutoka uwanjani zinaonyesha kuwa Iran imetumia kipindi cha usitishaji mapigano kuimarisha tena uwezo wake wa kiulinzi. Inadaiwa kuwa majeshi ya Iran yamekarabati na kurejesha vifaa vya kijeshi, ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani na ghala za makombora zilizoharibiwa katika mashambulizi ya awali.
Hatua hizo zinaripotiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa gharama za kijeshi ambazo Marekani ingeweza kukabiliana nazo iwapo vita vingerejea.