Jerusalem —

Kwa mujibuwa gazeti la Jerusalem Post, Uhitaji wa huduma za afya ya akili nchini Israel umeongezeka kwa takriban asilimia 240 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Hali hii inachochewa na vita vinavyoendelea na athari zake mbaya za muda mrefu kisaikolojia kwa wananchi, kwa mujibu wa shirika la huduma za afya la Clalit (Clalit Health Services).

Shirika hilo, ambalo ni mtoa huduma mkubwa zaidi wa afya nchini humo linalohudumia zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote, lilitangaza ongezeko hilo la kutisha siku ya Jumatatu wakati wa ziara ya Kamati ya Afya ya Bunge (Knesset) katika Hospitali ya Clalit-Beilinson. Ili kukabiliana na wimbi hilo kubwa la wagonjwa, Clalit imeajiri wataalamu wapya 290 wa afya ya akili na kupanua wigo wa kliniki 40 za afya ya akili nchi nzima.

Takwimu hizi zinaangazia kile ambacho wataalamu wanakielezea kama “athari fiche za vita” — kiwewe cha kitaifa ambacho madhara yake yanavuka mbali zaidi ya majeraha ya kimwili. Tangu kuzuka kwa mzozo wa sasa, jamii ya Israel imekuwa ikikabiliwa na mawimbi ya mara kwa mara ya msongo wa mawazo kutokana na mashambulizi ya roketi, ukimbizi wa ndani, kupoteza maisha, na tishio la kiusalama la kudumu, mambo ambayo yamechangia ongezeko kubwa la matatizo ya wasiwasi (anxiety), sonona (depression), ugonjwa wa kiwewe baada ya tukio (PTSD), na mahitaji mengine ya kiakili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *