Iran imetangaza nia yake ya kushirikiana kwa karibu na nchi jirani ya Pakistan ili kuhakikisha usalama endelevu wa chakula katika ukanda wa Ghuba ya Uajemi.

Katika mazungumzo yaliyofanyika mjini Tehran kati ya Waziri wa Kilimo na Jihad wa Iran, Gholamreza Nouri Ghezeljeh, na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Syed Mohsin Naqvi, pande zote mbili zimesisitiza kuwepo kwa uwezo mkubwa wa kibiashara na uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo baina ya nchi hizo mbili.

Waziri Ghezeljeh amesema kuwa uhusiano wa kihistoria na kitamaduni kati ya Tehran na Islamabad ni msingi imara wa ushirikiano wa kimkakati. Ameongeza kuwa nchi hizo zimeanza kuweka misingi madhubuti ya kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za msingi, hatua inayotajwa kuwa ni mhimili mkuu wa usalama wa chakula kwa mataifa hayo na kanda nzima.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Syed Mohsin Naqvi, amekaribisha fursa hizo za ushirikiano. Hata hivyo, Naqvi amesisitiza kuwa amani na usalama ni vigezo muhimu vya lazima ili kuruhusu biashara na usalama wa chakula kustawi katika eneo hilo.

Katika mkutano huo, mawaziri hao wamekubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Rais Masoud Pezeshkian nchini Pakistan mwaka jana, hasa katika sekta ya kilimo na uboreshaji wa usafirishaji wa bidhaa muhimu za msingi.

Ushirikiano huu unatazamwa kama hatua muhimu ya kuimarisha uchumi na utulivu katika kanda ya Mashariki ya Kati na Asia ya Kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *