WASHINGTON — Sekta ya kilimo nchini Marekani inakabiliwa na mtikisiko mkubwa kufuatia wimbi jipya la kufilisika kwa mashamba, hali ambayo inatishia uwepo wa mashamba mengi ya kifamilia.

Wakulima wengi wananyooshea kidole sera za kiuchumi na mivutano ya kibiashara ya serikali ya Trump kuwa chanzo kikuu cha janga hili.Kwa mujibu wa takwimu mpya kutoka Shirikisho la Mashamba Marekani (American Farm Bureau Federation), maombi ya kufilisika yameshuhudia ongezeko la kutisha la asilimia 46% katika mwaka 2025, na kufikia jumla ya kesi 315.

Imebainika kuwa majimbo ya Midwest na Kusini mwa Marekani ndiyo yaliyoathirika zaidi na janga hili.

Ripoti zinaonyesha kuwa mashamba yaliyodumu kwa vizazi kadhaa sasa yapo ukingoni mwa kufungwa. Mfano halisi ni familia ya Nelson kutoka jimbo la Louisiana, inayomiliki takribani ekari 3,500 za ardhi, pamoja na mkulima Fate Sparrow wa jimbo la Georgia.

Wote kwa pamoja wanapitia kipindi kigumu cha kifedha kinachotishia shughuli zao. Akielezea ukubwa wa tatizo hilo, Bw. Sparrow ameeleza kuwa tayari amepata hasara inayokadiriwa kufikia dola 700,000.

Hali hii imemvunja moyo kiasi cha kusitisha mpango wake wa kumkabidhi mwanawe urithi wa shamba hilo la familia.

Aidha, amebainisha kuwa anawafahamu wakulima wengine kadhaa ambao tayari wamelazimika kuachana kabisa na kilimo.

Kwa upande wake, Willis Nelson kutoka Louisiana amefafanua kuwa mgogoro huu umechochewa na mambo kadhaa, ikiwemo vita vya kibiashara vilivyoifanya China kupunguza ununuzi wa soya kutoka Marekani.

Sababu nyingine ni kupanda kwa bei ya mbolea kutokana na kufungwa mlango wa Hormuz baada ya Marekani na Israel kuvamia Iran kijeshi, kushuka kwa bei za mazao sokoni, pamoja na urasimu unaofanya misaada ya serikali kuwafikia wakulima kwa kuchelewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *