PARIS – Mkuu wa Shirika la Nishati la Kimataifa (IEA) ametoa onyo kali mnamo tarehe 18 Mei, akieleza kuwa hifadhi za kibiashara za mafuta duniani zimesaliwa na kiasi kinachoweza kutosheleza kwa wiki chache pekee.
Hali hii inatokana na kupungua kwa kasi kwa akiba hizo kufuatia vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, pamoja na kuendelea kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Akizungumza siku ya Jumatatu, Mkurugenzi Mtendaji wa IEA, Fatih Birol, alibainisha kuwa hatua ya kutoa mafuta kutoka kwenye akiba ya kimkakati imeongeza mapipa milioni 2.5 kwa siku katika soko, lakini alionya vikali kuwa akiba hizo “hazina ukomo.” “Hifadhi za kibiashara zinaweza kudumu kwa wiki kadhaa tu, lakini tunapaswa kufahamu wazi kuwa kiwango chake kinashuka kwa kasi sana,” aliongeza Birol.
Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao kwa kawaida hupitisha asilimia 20 ya mauzo yote ya mafuta duniani, umesalia kufungwa tangu kuanza kwa vita hivyo mnamo tarehe 28 Februari.
Kufungwa huko kumesababisha bei ya mafuta ghafi kupaa kwa kiasi kikubwa katika soko la kimataifa.Kukabiliana na hali hiyo, mnamo tarehe 11 Machi, shirika la IEA lilitangaza kuwa nchi zake wanachama 32 zilikubaliana kuingiza sokoni mapipa milioni 400 ya mafuta kutoka kwenye hifadhi zao za dharura ili kupunguza athari za uhaba uliozuka. Kufikia mapema mwezi Mei, tayari mapipa milioni 164 yalikuwa yameshatolewa.
Birol alitoa matamshi hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika kikao cha mawaziri wa fedha wa Kundi la Nchi Saba (G7) kilichofanyika mjini Paris.
Zaidi ya hayo, alieleza kuwa hifadhi za mafuta zinakabiliwa na shinikizo kubwa zaidi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya dizeli, mbolea, mafuta ya ndege, na petroli. Ongezeko hili la mahitaji linachangiwa sana na kuanza kwa msimu wa kilimo wa masika na msimu wa usafiri wa majira ya joto katika nchi za kizio cha kaskazini (northern hemisphere).
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi punde ya kila mwezi ya soko la mafuta iliyotolewa na IEA, hifadhi za mafuta duniani zilipungua kwa kiwango cha kihistoria cha mapipa milioni 246 katika miezi ya Machi na Aprili.a