Falme za Kiarabu (UAE) zimetoa dola milioni 100 kwa taasisi inayoungwa mkono na Marekani ijulikanayo kama “Board of Peace” kwa ajili ya kufadhili mafunzo ya kikosi kipya cha polisi wa Palestina kitakachopelekwa katika Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia.
Kwa mujibu wa ripoti, huu ndio mchango mkubwa zaidi kuwahi kupokelewa na bodi hiyo, baada ya wanachama wake tisa kuahidi awali jumla ya dola bilioni 7. Marekani pia ilitangaza uwekezaji wa dola bilioni 10 katika mkutano wa wafadhili uliofanyika Februari mwaka huu.
Vyanzo vya kidiplomasia vinaeleza kuwa waajiriwa wapya watafundishwa nchini Misri na Jordan. Kampuni ya usalama kutoka UAE imepewa jukumu la kuunda kikosi cha takribani maafisa 27,000 watakaohudumu Gaza.
Ripoti ya awali ilisema kuwa Wapalestina waliowahi kufanya kazi kama watumishi wa umma katika Ukanda wa Gaza wataruhusiwa kuomba kujiunga na kikosi hicho kipya, hata hivyo watapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kiusalama na mamlaka za Israel kabla ya kuidhinishwa.
Hata hivyo, Israel imeripotiwa kuendelea kushambulia vikosi vya polisi vya Gaza licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Oktoba. Katika tukio la hivi karibuni lililoripotiwa Jumatano, afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Palestina aliuawa.
Takwimu zinaonyesha kuwa tangu kusitishwa kwa mapigano tarehe 10 Oktoba, Wapalestina wasiopungua 837 wameuawa, na kufanya idadi ya waliopoteza maisha kufikia zaidi ya 72,000 tangu kuanza kwa mapigano.
Wakati huo huo, Ali Shaath, aliyechaguliwa kuongoza Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Gaza (NCAG), amesema kuwa mchakato wa kuajiri polisi tayari umeanza. Ameeleza kuwa hali ya Gaza bado ni tete kutokana na uharibifu mkubwa wa miundombinu na mahitaji makubwa ya kibinadamu.Kikosi hicho kipya cha polisi kitafanya kazi chini ya usimamizi wa NCAG, chombo cha mpito cha utawala wa kiteknokrati wa Palestina.
Aidha, mpango wa Marekani wa vipengele 20 uliopendekezwa mwezi Septemba unapendekeza kuundwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Ustawi (ISF) kitakachoshirikiana na polisi wa Palestina waliopata mafunzo mapya ili kusaidia kuleta utulivu katika Ukanda wa Gaza.