Crystal Palace imefanikiwa kutinga fainali ya Ligi ya Mkutano Ulaya baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Shakhtar Donetsk ya Ukraine katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali uliochezwa Alhamisi.
Timu hiyo ya England ilionyesha ubora wake tena baada ya pia kushinda mchezo wa kwanza kwa mabao 3-1, hivyo kufuzu kwa jumla ya mabao 5-2 katika michezo yote miwili.
Katika mchezo huo, bao la kwanza la Crystal Palace lilipatikana dakika ya 25 kufuatia Pedro Henrique wa Shakhtar kujifunga.
Ismaïla Sarr aliiongezea Palace bao la pili dakika ya 52 na kuimarisha matumaini ya timu hiyo kufuzu.Shakhtar Donetsk walipata bao lao pekee dakika ya 34 kupitia kwa Eguinaldo, lakini halikutosha kuizuia Crystal Palace kusonga mbele hadi hatua ya fainali.
Kwa ushindi huo, Crystal Palace sasa itakutana na Rayo Vallecano ya Hispania katika fainali ya michuano hiyo, itakayochezwa tarehe 27 Mei mjini Leipzig, Ujerumani.