DAR ES SALAAM, Julai 16 – Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema Serikali inaendelea na uchunguzi kuhusu kutoweka kwa mwanasiasa Humphrey Polepole, huku akisisitiza kuwa uchunguzi wa aina hiyo unahitaji muda ili kuhakikisha ukweli unabainika na haki inatendeka kwa wote.
Kauli ya Katambi imekuja ikiwa ni siku 274 tangu Polepole aripotiwe kutoweka alfajiri ya Jumatatu, Oktoba 16, 2025, akiwa katika makazi yake ya Ununio, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahojiano maalum na AyoTV, Katambi alisema matukio mengi yanayodaiwa kuwa ya utekaji yamekuwa yakihusishwa na Serikali, lakini baadaye uchunguzi umeonyesha baadhi yake yalitokana na migogoro binafsi kati ya raia.
“Kulikuwa na matukio ambayo watu walidai Serikali imehusika, lakini baadaye ikabainika si kweli. Serikali haiteki watu; Serikali inawakamata kwa mujibu wa sheria na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa hata pale ambapo baadhi ya watumishi wa Serikali au askari wamehusika kufanya makosa kwa kutumia mamlaka yao vibaya, hatua za kisheria zimekuwa zikichukuliwa dhidi yao.
“Sisemi kwamba natetea Serikali. Wapo askari ambao wamebainika kufanya makosa na wamechukuliwa hatua. Lakini hilo halimaanishi kwamba Serikali ndiyo inayotekeleza vitendo hivyo,” aliongeza.
Akizungumzia suala la Polepole, Katambi alisema taarifa ya mwisho iliyotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama ni kwamba uchunguzi na upelelezi bado unaendelea. Alieleza kuwa kumekuwa na taarifa zinazokinzana kuhusu mahali alikokuwa Polepole baada ya kutoweka, jambo linalohitaji uchunguzi wa kina.
“Kulikuwa na taarifa zikisema inasadikika hakuwepo nchini, lakini pia zipo taarifa zinazosema alikuwa nchini. Kama ni kweli au si kweli, upelelezi unaendelea,” alisema.
Kauli ya Waziri inamaanisha kuwa hadi sasa hakuna hitimisho rasmi kuhusu mazingira ya kutoweka kwa Humphrey Polepole. Serikali imeeleza kuwa uchunguzi utaendelea hadi ukweli utakapobainika na taarifa rasmi kutolewa kwa umma.
