Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ameagiza kufungwa kwa runinga za NTV Uganda na Spark TV zinazomilikiwa na Nation Media Group (NMG), akieleza kutoridhishwa kwake na namna vyombo vya habari vinavyofanya kazi nchini humo.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Jenerali Muhoozi alisema kuwa haamini katika kile alichokiita uhuru usio na mipaka wa vyombo vya habari, akisisitiza kuwa taasisi za habari zinapaswa kuongozwa kwa misingi ya kile alichokiita “mageuzi” na nidhamu katika utoaji wa taarifa.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Muhoozi kuonya hapo awali kwamba alikuwa akisubiri idhini ya Rais Yoweri Museveni, ambaye pia ni babake, kabla ya kuchukua hatua dhidi ya vyombo hivyo vya habari. Kauli zake zilionyesha kuwa serikali ilikuwa na wasiwasi kuhusu namna baadhi ya vyombo vya habari vinavyoripoti masuala ya kisiasa na ya serikali.

Usiku wa kuamkia Jumapili, vikosi vya usalama vilivamia ofisi za NTV Uganda na Spark TV zilizoko Namuwongo na katika eneo la Hoteli ya Serena jijini Kampala. Wafanyakazi wa vituo hivyo walizuiwa kuingia kazini huku matangazo yakisitishwa ghafla.

Katika ujumbe wake mmoja, Muhoozi aliandika kwamba NTV na Monitor zitafungwa kuanzia siku hiyo na hazitafunguliwa tena bila idhini yake. Kauli hiyo ilionyesha msimamo mkali wa jeshi kuhusu udhibiti wa vyombo vya habari vinavyodhaniwa kutofuata mwelekeo unaotakiwa na mamlaka.

Hata hivyo, kufungwa kwa vituo hivyo kumeibua ukosoaji kutoka kwa mashirika ya wanahabari katika eneo la Afrika Mashariki. Muungano wa Wanahabari nchini Kenya na Muungano wa Wanahabari Afrika Mashariki wamesema hatua hiyo inaibua maswali kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na utawala wa sheria nchini Uganda.

Mashirika hayo yametaka serikali ya Uganda kueleza wazi sababu za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya vyombo hivyo vya habari iwapo kweli kulikuwa na sheria zilizokiukwa. Pia yamesisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa wanahabari na kutafuta suluhu ya migogoro kati ya serikali na vyombo vya habari katika ukanda huo.

Leave a Reply