TEL AVIV/RIYADH – Ripoti mpya iliyotolewa na vyombo vya habari vya Israel, ikinukuu taarifa kutoka gazeti la Haaretz, imefichua kuwepo kwa ushirikiano wa siri wa kijeshi kati ya Israel na nchi za Ghuba, licha ya kutokuwepo kwa uhusiano rasmi wa kidiplomasia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kampuni kubwa za ulinzi za Israel, Elbit Systems na Israel Aerospace Industries (IAI), zinadaiwa kuingia mikataba ya thamani ya mamilioni ya shekeli na Saudi Arabia pamoja na Qatar. Mikataba hiyo inahusisha uuzaji wa mifumo ya kisasa ya ulinzi wa makombora na vipuri muhimu kwa ajili ya ndege za kivita aina ya F-15.

Ufichuzi huo unaashiria kuwepo kwa mtandao wa kibiashara na kiulinzi unaoendelea nyuma ya pazia. Aidha, ripoti hiyo imedai kuwa Qatar imejipatia vifaa maalum vya ulinzi kutoka Elbit Systems kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa viongozi wake wa ngazi ya juu. Serikali za nchi hizo husika bado hazijatoa tamko rasmi kuhusu madai hayo yanayoashiria mabadiliko ya kimkakati katika usalama wa kanda hiyo.

Leave a Reply