NAIROBI, KENYA
Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, amezua mjadala mzito nchini humo baada ya kutoa tamko kali la hadharani dhidi ya kampuni ya habari ya Standard Group, akishutumu kile alichokiita kuwa ni mkakati wa makusudi wa kumchafua yeye na serikali yake.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), kiongozi huyo wa nchi ameonekana kupandwa na ghadhabu kufuatia mfululizo wa vipindi vinavyopeperushwa na kituo cha televisheni cha KTN News. Vipindi hivyo vimekuwa vikiangazia miradi ya serikali inayodaiwa kukwama pamoja na ahadi za kisiasa ambazo hazijatimizwa tangu aingie madarakani.
Katika ujumbe wake ambao umejaa lugha ya hisia kali, Rais Ruto alimuhutubia moja kwa moja mmiliki wa kampuni hiyo, Gideon Moi (GMoi), akidai kuwa mfululizo huo wa taarifa ni “propaganda za ulaji njama” zenye lengo la kumshurutisha ili atoe upendeleo fulani.
“G-Moi, vichwa vya habari vya propaganda vya kampuni yako ya Standard vinavyoendeshwa siku tano kwa wiki dhidi yangu na rekodi ya mabadiliko ya serikali yangu, havitakupa chochote na haviendi popote,” aliandika Rais Ruto.
Rais aliendelea mbele zaidi kwa kusema kuwa hatakubali kamwe kutishwa (blackmail) ili kutosheleza kile alichokiita “uroho” wa watu wachache, akisisitiza kuwa Kenya ni mali ya Wakenya wote na si ya mtu mmoja.
Katika kile kinachoonekana kama changamoto ya wazi kwa chombo hicho cha habari, Rais Ruto alihitimisha kwa kusema: “Jaribuni hata siku nane kwa wiki. Fanyeni lolote mnavyoweza (Do your worst).”
Hali hii imetafsiriwa na wachambuzi wa mambo kama mwendelezo wa uhusiano wenye msukosuko kati ya serikali ya sasa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya, huku kukiwa na hofu ya kuingiliwa kwa uhuru wa habari. Hadi sasa, uongozi wa Standard Group haujatoa jibu rasmi kufuatia mashambulizi hayo ya Rais.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Ruto na viongozi wa ngazi za juu wa serikali yake kuvinyoshea kidole vyombo vya habari, wakidai kuwa vinatumika na wapinzani wa kisiasa kupotosha umma kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini humo.