WASHINGTON/JERUSALEM – Ripoti mpya kutoka kwa shirika la habari la Axios imefichua mivutano ya chinichini iliyopelekea Israel kusitisha mpango wake wa awali wa kutekeleza mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya nchi ya Iran.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, awali Israel ilikuwa imekamilisha maandalizi ya wimbi kubwa la mashambulizi dhidi ya Iran, hali ambayo ingetishia kuingiza eneo lote la Mashariki ya Kati katika vita kamili. Hata hivyo, mpango huo ulizimwa ghafla kufuatia mazungumzo ya simu kati ya Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Onyo la Moja kwa Moja
Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa katika mazungumzo hayo, Trump alitoa onyo la wazi na kali kwa Netanyahu akimstahadharisha kuhusu hatari ya kuendelea na mashambulizi hayo bila tahadhari.
Trump ananukuliwa akisema: “Bibi, ni bora uwe mwangalifu, la sivyo utajikuta peke yako hivi karibuni” (Bibi, you better be careful, or you will be on your own very soon). Onyo hilo lilitafsiriwa kama ishara kuwa Marekani inaweza kuondoa ulinzi au msaada wake wa kidiplomasia na kijeshi ikiwa Israel itachochea vita vikubwa zaidi.
Makubaliano ya Kusitisha Mapigano
Kufuatia shinikizo hilo kutoka kwa Trump, Netanyahu anaripotiwa kulegeza msimamo wake na kukubali kusitisha mashambulizi hayo yaliyokuwa yamepangwa.
Hata hivyo, Netanyahu ameweka sharti moja kuu: Israel itasitisha harakati hizo mradi tu Iran nayo iache mara moja mashambulizi yake dhidi ya maeneo ya Israel. Hatua hii inaonekana kama juhudi za kuzuia mlipuko wa vita ambao ungetikisa usalama wa dunia na soko la nishati kimataifa.
Hadi sasa, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel haijatoa tamko rasmi kuhusu maelezo hayo ya simu yaliyofichuliwa na Axios.