SANA’A, YEMEN – Msemaji wa Jeshi la Yemen, Yahya Saree, ametangaza rasmi kuzuia harakati zote za meli za Israel katika Bahari ya Shamu, akisisitiza kuwa marufuku hiyo inaanza kutekelezwa mara moja.

Katika taarifa yake iliyosheheni ujumbe mzito, Yahya Saree amebainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na uvamizi wa Marekani na Uzayuni dhidi ya mataifa ya Iran, Palestina, Lebanon, Iraq, na Yemen. Amesema hatua hiyo inalenga kudhoofisha mradi wa “Israel Kuu” na kuvunja mzingiro wa kidhalimu uliowekwa na Marekani dhidi ya wananchi wa Gaza, Lebanon, Iran, na Yemen.

Mashambulizi ya Makombora Katika Eneo la Jaffa
Pamoja na marufuku hiyo ya baharini, msemaji huyo amethibitisha kuwa vikosi vya Yemen vimefanya operesheni ya kijeshi kwa kushambulia shabaha nyeti katika eneo la Jaffa (Tel Aviv) linalokaliwa kwa mabavu. Operesheni hiyo imetekelezwa kwa kutumia mfululizo wa makombora ya kisasa.

Onyo Kali kwa Adui
Akitoa onyo kwa upande wa Israel, Saree alisema:
“Tunatangaza marufuku kamili na ya kudumu kwa usafiri wa baharini wa adui Muisraeli katika Bahari ya Shamu. Kuanzia wakati huu wa kutangazwa kwa taarifa hii, harakati yoyote ya adui itachukuliwa kama lengo halali la kijeshi la vikosi vyetu.”

Jeshi la Yemen limesisitiza kuwa litajibu mapigo kwa kiwango cha juu zaidi na kwamba operesheni zao za kijeshi zitaongezeka kulingana na hali ya mapambano yanavyoendelea katika mhimili wa upinzani na jihadi.

Taarifa hii inaashiria kuongezeka kwa taharuki katika njia hiyo muhimu ya kibiashara duniani, huku Yemen ikionyesha nia ya dhati ya kuendeleza operesheni zake kuunga mkono washirika wake katika kanda hiyo.

Leave a Reply