Tel Aviv/Tehran — Ujasusi wa Israel umetathmini kuwa Iran ilihamisha maelfu ya mashine za kurutubisha urani (nuclear centrifuges) kwenda katika eneo la Mlima Pickaxe, kituo cha nyuklia kilicho chini ya ardhi na chenye ulinzi mkali karibu na Natanz.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Israel iliifahamisha Marekani kuwa taarifa zake za kijasusi zinaonyesha uhamishaji huo ulifanyika mwishoni mwa mwaka uliopita, baada ya vita vya siku 12 mnamo Juni 2025, ambapo Marekani ilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran kwa kutumia ndege za mabomu aina ya B-52.
Taarifa hiyo haijaeleza idadi kamili ya mashine zilizohamishwa wala kutoa ushahidi wa wazi unaothibitisha madai hayo.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa sehemu ya juhudi za Iran kulinda miundombinu yake ya nyuklia dhidi ya mashambulizi yanayoweza kutokea, huku suala la mpango wa nyuklia wa Tehran likiendelea kuwa chanzo cha mvutano kati ya Iran, Israel na Marekani.