Wakati ngoma ya vita ikiendelea kurindima katika Mlango-bahari wa Hormuz, diplomasia ya dharura imeanza kuchukua mkondo mpya. Pakistan na Qatar zimejitokeza na mpango wa dharura wa kuziokoa Washington na Tehran kutoka kwenye janga la vita kamili ambavyo hakuna upande uliojiandaa kuvihimili.
Mataifa ya Pakistan na Qatar yamewasilisha pendekezo la pamoja la kuzitaka Iran na Marekani kurejea katika nafasi zao za kabla ya tarehe 9 Julai kama hatua ya kwanza ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo. Sambamba na hayo, shirika la habari la Reuters, likimnukuu afisa mmoja wa Iran, limeripoti kuwa wapatanishi wamependekeza makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku 10 ili kutoa nafasi ya kujadili njia za kufufua “Mkataba wa Maelewano wa Islamabad.”
Hatua hii ya Qatar na Pakistan si ya bahati mbaya; inatokana na hofu ya kiuchumi na kiulinzi. Mlango-bahari wa Hormuz ukiwa hauna usalama, uchumi wa mataifa ya Ghuba na usafirishaji wa nishati kwenda Asia Kusini unatikisika. Kwa upande wa Marekani, pendekezo hili linakuja kama njia ya dharura ya kutokea (off-ramp) baada ya ripoti za Pentagon kufichua upungufu mkubwa wa akiba ya makombora na mifumo ya ulinzi wa anga. Hata hivyo, kurudi kwenye msimamo wa kabla ya Julai 9 kutalazimisha pande zote mbili kukubali makubaliano mapya ya ugawanaji madaraka ya usafiri wa baharini.
Uwezo wa kijeshi wa Marekani uko hatarini. Ripoti mpya kutoka kwa The Telegraph imeibua swali zito: Je, Washington ina rasilimali za kutosha za kuendeleza vita vikubwa dhidi ya Iran? Jibu, kwa mujibu wa maafisa wa Pentagon, linaashiria udhaifu mkubwa wa kimkakati.