Washington, Marekani — Rais wa Marekani Donald Trump amesema anasikitishwa na kifo cha wanajeshi wawili wa Marekani waliouawa nchini Jordan, huku akisisitiza kuwa Iran haitakiwi kumiliki silaha za nyuklia. Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Washington na Tehran ukiendelea kuongezeka baada ya Iran kutangaza kusitisha baadhi ya ahadi zake chini ya makubaliano ya muda.
Akizungumza na waandishi wa habari, Trump alisema vifo hivyo ni jambo la kusikitisha na kuwapongeza wanajeshi hao kwa huduma yao kwa taifa.
“Tunachukia kuona jambo hili likitokea. Wamefariki wakiwa katika huduma kwa nchi yetu,” Trump alisema.
Rais huyo wa Marekani hakutoa maelezo ya kina kuhusu mazingira ya tukio hilo, lakini alirudia msimamo wake kwamba Iran haipaswi kuwa na silaha za nyuklia.
“Iran haiwezi na haipaswi kuwa na silaha ya nyuklia,” alisema Trump.
Kauli hiyo imekuja baada ya taarifa za vifo vya wanajeshi wawili wa Marekani nchini Jordan, tukio lililoongeza shinikizo la kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati ambalo tayari limekuwa likikabiliwa na mvutano mkubwa kati ya Marekani na Iran.
Baadaye, baada ya Iran kutangaza kusitisha utekelezaji wa baadhi ya majukumu yake chini ya makubaliano ya muda, Baada ya Marekani kuvunja maagano hayo kwa kufanya mashambulizi Iran, Trump alionyesha kutokuwa na wasiwasi kuhusu hatua hiyo, akisema:
“Sijali kabisa,” akimaanisha uamuzi wa Tehran.
Hatua ya Iran imeelezwa kuwa ni majibu ya kile inachokitaja kama shinikizo la nje na hatua za upande mmoja zinazokiuka haki yake ya kufanya maamuzi huru kuhusu masuala yake ya kimkakati.
Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanaonya kuwa kuendelea kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili kunaweza kuongeza hatari ya mzozo mpana zaidi katika eneo ambalo tayari limeathiriwa na vita na migogoro ya muda mrefu.
Mzozo huu unaibua tena mjadala kuhusu usawa katika mfumo wa kimataifa, matumizi ya nguvu za kijeshi na haki ya mataifa kujitegemea katika kuamua sera zao za ndani na za kigeni bila shinikizo la mataifa yenye nguvu.
Kwa sasa, macho yanaelekezwa kwenye hatua zitakazochukuliwa na Washington na Tehran katika siku zijazo. Ikiwa njia za kidiplomasia zitapewa nafasi, kuna uwezekano wa kupunguza mvutano; lakini kuendelea kwa sera za mashinikizo na makabiliano kunaweza kuongeza hatari ya kuyumbisha zaidi usalama wa Mashariki ya Kati.