Abu Dhabi, Falme za Kiarabu (UAE) — Serikali ya Falme za Kiarabu imesema ina wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, ikitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama, kupunguza mivutano na kurejea kwenye mazungumzo ya kidiplomasia ili kuzuia hali kuzidi kuwa mbaya.
Katika taarifa yake, UAE imesisitiza umuhimu wa pande zote kuchukua tahadhari kubwa na kuepuka hatua zinazoweza kusababisha mzozo mpana zaidi katika eneo hilo lenye umuhimu mkubwa kwa usalama na uchumi wa dunia.
Miongoni mwa hatua ilizozitaka UAE ni kusitishwa kwa mapigano mara moja, kuonyeshwa kwa kiwango cha juu cha kujizuia na kurejeshwa kwa njia za mazungumzo kama suluhisho la kupunguza tofauti zilizopo.
Serikali hiyo pia imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha usafirishaji salama na usiokatizwa kupitia Mlango wa Hormuz, ikieleza kuwa njia hiyo ni muhimu kwa uchumi wa dunia kutokana na nafasi yake katika usafirishaji wa nishati na biashara ya kimataifa.
“Usalama na uhuru wa usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz ni jambo muhimu kwa uthabiti wa uchumi wa dunia,” UAE imesisitiza katika msimamo wake.
Aidha, Abu Dhabi imeonya dhidi ya mashambulizi yanayolenga miundombinu ya kiraia kama shule, hospitali, mitambo ya kusafisha maji na vituo vya nishati, ikisema vitendo hivyo ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na haviwezi kuhalalishwa kwa sababu yoyote.