Dkt Oburu Oginga

NAIROBI — Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Dkt Oburu Oginga, bado yuko Uingereza ambako anaendelea kufuatiliwa na madaktari, huku familia yake ikisema hali yake imeimarika.

Dadake, Mwakilishi wa Wanawake wa Kisumu Ruth Odinga, amesema familia haina mpango wa haraka wa kumrejesha Kenya hadi madaktari wakamilishe ukaguzi na miadi yake.

“Ameimarika sana, lakini hatujapanga kurejea kwake Kenya kwa sasa,” amesema Ruth.

Amefafanua kuwa Dkt Oginga, mwenye umri wa miaka 83, hajalazwa hospitalini, bali anaishi karibu na kituo anachopokea huduma ili kurahisisha miadi yake na madaktari.

Wakati akiendelea kukaa Uingereza, Dkt Oginga pia amekuwa akishiriki baadhi ya shughuli kwa njia ya mtandao. Wiki hii alisema yeye na mkewe, Mama Judy, walikutana na Balozi wa Kenya nchini Uingereza, Maurice Makoloo, na kujadili uhusiano wa Kenya na Uingereza pamoja na masuala yanayowahusu Wakenya wanaoishi ughaibuni.

Maoni