Wizara ya Afya nchini Kenya imethibitisha kisa cha kwanza cha Ebola, kikihusisha raia wa Kenya aliyekuwa akiishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kabla ya kusafiri hadi Nairobi kupitia Uganda.
Waziri wa Afya, Aden Duale, amesema mgonjwa huyo alifariki Jumatatu baada ya kuugua, huku mamlaka za afya zikianza ufuatiliaji wa watu waliowahi kuwa karibu naye.
Kwa mujibu wa wizara, hadi sasa watu 28 waliokuwa na mawasiliano ya karibu na mgonjwa huyo wametambuliwa na wanaendelea kufuatiliwa na wataalamu wa afya.
Mamlaka pia zinaendelea kuwatafuta watu wengine 27 ambao walikuwa katika safari moja na mgonjwa huyo wakati akisafiri kuelekea Nairobi.
Wizara ya Afya imesema juhudi za ufuatiliaji na udhibiti wa maambukizi zinaendelea, huku wananchi wakitarajiwa kupewa taarifa zaidi kadri uchunguzi unavyoendelea.
Chanzo: Wizara ya Afya Kenya.