Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amesisitiza kuwa nchi yake lazima ipate njia ya kuelekea Bahari Nyekundu, huku mvutano wa kisiasa na kijeshi katika Pembe ya Afrika ukiendelea kuongezeka.
Abiy ametoa kauli hiyo wakati akianza muhula mwingine wa miaka mitano, akisema upatikanaji wa bandari ni suala muhimu kwa maendeleo na mustakabali wa Ethiopia, ambayo haina pwani tangu Eritrea ilipopata uhuru mwaka 1993.
Amesema Ethiopia itafuata kanuni ya “kutoa na kupokea” katika juhudi zake za kupata njia ya baharini na kusisitiza kuwa Addis Ababa itaendelea kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Misri, Eritrea, Somalia na Sudan kusisitiza kuwa usimamizi wa Bahari Nyekundu unapaswa kubaki mikononi mwa nchi zilizo na mwambao katika bahari hiyo.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amesema nchi yake haipingi Ethiopia kutumia bandari za Somalia, lakini amesisitiza kuwa suala hilo linapaswa kushughulikiwa kupitia mazungumzo rasmi kati ya serikali mbili.
Mvutano kuhusu bahari unakuja wakati Ethiopia pia ikikabiliwa na mapigano mapya kaskazini mwa nchi na uhusiano wake na Eritrea ukiwa umedorora kwa kiwango kikubwa.
Vyanzo: Al Jazeera, AFP, AP.
