Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa agizo la kupunguza huduma za mawasiliano ya satelaiti zinazotumiwa na Jeshi la Ukraine katika operesheni za kijeshi na shughuli za droni limetoka Ikulu ya Marekani.
Kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa na Reuters, maafisa waandamizi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani wamepokea maelekezo ya kupunguza huduma za Starshield, mfumo wa satelaiti wenye uwezo wa kijeshi unaotolewa na kampuni ya SpaceX. Pentagon inatajwa kuwa mteja mkubwa zaidi wa mfumo huo.
Hatua hiyo inaripotiwa wakati maafisa wa Ukraine wakieleza kuwa baadhi ya vifaa vya Starlink vinavyotumika kijeshi vimeacha kufanya kazi, hali iliyovuruga operesheni za droni. Starshield ni huduma ya kijeshi inayohusiana na teknolojia ya Starlink, lakini mifumo hiyo si kitu kimoja.
Reuters imehusisha muda wa hatua hiyo na shinikizo la Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa Ukraine kusitisha mashambulizi dhidi ya viwanda vya kusafisha mafuta nchini Urusi.
Chanzo: Tasnim News, ikinukuu Reuters.

Maoni