Mvutano wa kidiplomasia umeibuka kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kufuatia mazungumzo ya simu yaliyotajwa kuwa ya “taharuki” siku ya Jumanne, kuhusu juhudi mpya za kufikia makubaliano na taifa la Iran.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na mtandao wa Axios, viongozi hao wawili wameshindwa kufikia mwafaka kuhusu mwelekeo wa sera za kigeni kuelekea Tehran. Rais Trump amemuarifu Waziri Mkuu Netanyahu kuwa wapatanishi wako katika hatua za mwisho za kuandaa “barua ya dhamira” (letter of intent). Hati hiyo inatarajiwa kusainiwa na Marekani na Iran ili kuhitimisha rasmi uhasama wa kivita na kuanzisha kipindi cha siku 30 cha mazungumzo ya kina.

Mada kuu za mazungumzo hayo zinatajwa kuwa ni mpango wa nyuklia wa Iran pamoja na kufunguliwa tena kwa njia muhimu ya maji ya Mlango-Bahari wa Hormuz.

Hata hivyo, Netanyahu amedhihirisha kupinga waziwazi mpango huo, akielezea shaka yake kubwa kuhusu nia ya Iran. Badala yake, kiongozi huyo wa Israel anasisitiza umuhimu wa kuendeleza operesheni za kijeshi ili kuendelea kusambaratisha miundombinu na uwezo wa kijeshi wa Iran.

Vyanzo vya karibu vilivyoshuhudia hali ya Netanyahu baada ya mazungumzo hayo, vimeelezea kuwa Waziri Mkuu huyo alikuwa amejawa na hasira kali kutokana na msimamo wa Trump.

Wakati huo huo, taarifa zinaarifu kuwa Netanyahu anafanya juhudi za kutafuta ziara ya kikazi mjini Washington katika wiki zijazo, ili kufanya mazungumzo ya uso kwa uso na Rais Trump kwa matumaini ya kuishawishi Marekani kubadili msimamo wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *