Rais wa Ufilipino, Ferdinand Marcos Jr, amebainisha kuwa nchi yake “haina chaguo” lingine ila kuhusika iwapo mzozo wa kijeshi utazuka katika kisiwa cha Taiwan.
Akizungumza katika mahojiano maalum na vyombo vya habari vya Japani, kiongozi huyo alisisitiza kuwa uamuzi huo unatokana na sababu za kijiografia na usalama wa raia wake.
“Nchini Ufilipino, hatuna budi kwa sababu Taiwan iko karibu sana nasi. Pia, tuna takriban raia 200,000 wa Ufilipino wanaoishi na kufanya kazi nchini Taiwan,” alisema Rais Marcos Jr.
Kauli hii ya Rais imetolewa ikiwa ni maandalizi ya ziara yake rasmi mjini Tokyo wiki ijayo. Katika ziara hiyo, Rais Marcos anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Japani kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi na usalama wa kikanda, hatua inayotajwa na wachambuzi kama sehemu ya kukabiliana na ushawishi wa China.
Chini ya uongozi wa Marcos, Ufilipino imeendelea kudumisha uhusiano wake wa karibu na Marekani. Wakati huo huo, hali ya kisiasa nchini humo inazidi kupamba moto huku kiongozi wa upinzani anayeonekana kuwa na urafiki na Beijing, Sara Duterte, akikabiliwa na kesi ya kumwondoa madarakani (impeachment). Duterte anatajwa kuwa mshindani mkuu katika kinyang’anyiro cha urais wa mwaka 2028.
Mbali na changamoto za kijiopolitiki, serikali ya Manila inakabiliwa na shinikizo kubwa la kiuchumi kutokana na kizuizi cha nishati kinachoendelea katika Mlango-bahari wa Hormuz, hali inayotishia utulivu wa nishati nchini humo.