FBI Yatoa Zawadi ya Dola 200,000 kwa Taarifa Kuhusu Monica Witt
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) limetangaza zawadi ya dola 200,000 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa Monica Witt, aliyekuwa mtaalamu wa ujasusi katika Jeshi la Anga la Marekani, anayesakwa kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa niaba ya Iran.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, FBI ilisema bado inaendelea na juhudi za kumtafuta Witt, ambaye inaaminika alikimbilia Iran mwaka 2013.
Kwa mujibu wa shirika hilo, kuna uwezekano kuwa bado anaendelea kusaidia shughuli za kijasusi za Iran.
Daniel Wierzbicki, wakala maalum anayesimamia Kitengo cha Kupambana na Ujasusi na Uhalifu wa Mtandao katika Ofisi ya FBI ya Washington, alisema kuwa FBI inaamini kuna watu wanaoweza kuwa na taarifa kuhusu alipo Witt.
Alisisitiza kuwa shirika hilo linaendelea kuomba ushirikiano wa umma ili kumkamata na kumfikisha mbele ya sheria.
Monica Witt aliwahi kuwa afisa wa kupambana na ujasusi katika Ofisi ya Uchunguzi Maalum ya Jeshi la Anga la Marekani.
Kati ya mwaka 2003 na 2008, alifanya kazi katika majukumu ya kupambana na ujasusi yaliyompeleka katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.Mwaka 2019, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani wa wakati huo, John Demers, alidai kuwa Witt alishawishiwa na kuajiriwa na Iran. Baada ya kukimbilia nchini humo, inadaiwa alifichua taarifa nyeti ikiwa ni pamoja na uwepo wa mpango wa siri wa kukusanya taarifa za kijasusi na pia utambulisho wa afisa mmoja wa ujasusi wa Marekani, jambo lililoweka maisha ya afisa huyo hatarini.
Kulingana na hati ya mashtaka, kati ya Januari 2012 na Mei 2015, Witt alishirikiana na raia wa Iran kutoa nyaraka na taarifa zinazohusiana na ulinzi wa taifa wa Marekani, akiamini kuwa taarifa hizo zingetumika kuidhuru Marekani na kuipa faida Iran.
Hati hiyo pia inaeleza kuwa baada ya kukimbilia Iran, maafisa wa serikali ya nchi hiyo walimpatia Witt makazi pamoja na vifaa vya kompyuta ili kumwezesha kuendelea na shughuli zake.
Aidha, Wairani wanne pia wameshtakiwa katika kesi hiyo kwa makosa ya kula njama, kujaribu kufanya udukuzi wa kompyuta na wizi wa utambulisho uliokithiri.