Ripoti mpya iliyochapishwa na gazeti la La Tribune la Ufaransa imeonya kuhusu hatari ya upungufu wa dawa barani Ulaya, hali inayohusishwa na kuvurugika kwa mnyororo wa usambazaji wa sekta ya dawa duniani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sekta ya dawa barani Ulaya inategemea kwa takribani asilimia 80 uzalishaji kutoka China na India. Hata hivyo, ongezeko la bei ya mafuta na gesi limeifanya sekta hiyo kukumbwa na changamoto kubwa za uzalishaji na usafirishaji.
Aidha, kupungua kwa safari za ndege katika maeneo ya Mashariki ya Kati na Asia kumeelezwa kuwa moja ya sababu zinazochangia kucheleweshwa kwa usafirishaji wa malighafi na bidhaa za dawa kwenda Ulaya.
Kampuni ya bima ya biashara ya kimataifa, Coface, imeonya kuwa dawa kama asetaminofeni pamoja na aina kadhaa za antibiotiki ziko katika hatari kubwa ya upungufu. Ripoti hiyo inaeleza kuwa hata dawa zinazouzwa kwa bei ndogo sana hutegemea kwa kiasi kikubwa bidhaa zitokanazo na mafuta katika mchakato wa uzalishaji.
Wataalamu wanaonya kuwa iwapo shinikizo katika mfumo huu wa uzalishaji na usambazaji litaendelea, si tu kwamba bei za dawa zitaongezeka, bali pia baadhi ya malighafi muhimu zinaweza kupatikana kwa shida au kutopatikana kabisa.