Rais wa Kenya, William Ruto, ametoa wito kwa Afrika kupewa uanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, takwa ambalo limeungwa mkono na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.Rais William Ruto ametoa wito huo katika mkutano wa kilele wa Afrika na Ufaransa unaofanyika jijini Nairobi.Ruto amesema: “Afrika inapaswa kuwa na mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,” na ni wakati wa Umoja wa Mataifa kutambua bila kuchelewa kwamba Afrika haipaswi kukabiliwa na maamuzi ambayo haishirikishwi kuyachukuwa. Rais Ruto amesema ukosefu wa haki unaoshuhudiwa katika mfumo wa kimataifa unaimarisha mgawanyiko, na ametoa wito wa kufanyika mageuzi ya mfumo wa kitaasisi wa Umoja wa Mataifa kama haja ya kimkakati.Rais wa Kenya amesisitiza kwamba Afrika inataka kuondokana na utegemezi, kuwa na nafasi kubwa na kuwa mshirika kamili katika ngazi ya soko, kutokana na kuwa na kundi kubwa la vijana watanashati.Pia ametoa wito kwa nchi za Afrika kuhimiza uwekezaji wa kitaifa na ushirikiano wa kimkakati wa kimataifa, na akasema ni muhimu kwa Afrika kurekebisha mifumo yake, kwa sababu Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa pekee haziwezi kutimiza malengo ya ustawi katika bara hilo.Viongozi kutoka nchi zaidi ya 30 akiwemo Rais Emannuel Macron wa Ufaransa wanashiriiki katika mkutano wa Nairobi unaojadili amani na usalama, kuimarisha uwekezaji endelevu, kurekebisha mfumo wa fedha wa kimataifa, pamoja na mabadiliko katika sekta ya nishati na kuunganisha vipaumbele vya Afrika ndani ya mifumo ya uchumi wa dunia.Mkutano huo pia unachunguza njia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi za Afrika na Ufaransa, pamoja na kushughulikia changamoto zinazohusiana na ustawi, mabadiliko ya kidijitali, na mada zingine.Mkutano wa kilele wa Ufaransa na Afrika unafanyika katika kivuli cha changamoto kubwa zinazoikabili Ulaya, zinazotokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na athari zake ambazo zimeathiri dunia nzima.