New York Times imeripoti kuwa Bahari ya Caspian imekuwa njia muhimu ya kimkakati kwa Iran na Urusi katika kipindi cha mvutano wa kikanda na shinikizo la Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Urusi imekuwa ikitumia njia ya Bahari ya Caspian kusafirisha bidhaa za kijeshi na kibiashara kwenda Iran, huku ikiendelea kuiunga mkono Tehran dhidi ya mashambulizi na vikwazo vya Marekani.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa Bahari ya Caspian sasa ni njia muhimu ya kukwepa vikwazo na mzingiro wa Marekani katika Mlango wa Hormuz. Maafisa wa Marekani wanadai kuwa Urusi hutuma vipuri vya ndege zisizo na rubani (droni) kwenda Iran kupitia njia hiyo.

Aidha, bidhaa muhimu kama ngano, mahindi na mafuta ya kula ambazo hapo awali ziliingizwa kupitia njia za kimataifa, sasa zinapelekwa Iran kupitia bandari nne za nchi hiyo katika Bahari ya Caspian ili kuhakikisha usalama wa chakula wakati wa hali ya vita.

Kutokana na ukweli kwamba ni nchi tano pekee za mwambao wa Bahari ya Caspian zenye uwezo wa kufikia eneo hilo, na Marekani kutokuwa na nafasi ya kuingilia shughuli zake, eneo hilo limeelezwa kuwa mahali salama kwa usafirishaji wa kijeshi wa siri.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa baadhi ya meli huzima vifaa vyao vya ufuatiliaji wanapopita katika njia hiyo, jambo linalofanya uangalizi wa satelaiti kuwa mgumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *