Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Seyed Abbas Araghchi, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, wamefanya mazungumzo kwa simu Ijumaa jioni na kujadiliana kuhusu maendeleo muhimu ya kikanda.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alimweleza mwenzake wa Uturuki kuhusu hatua za hivi karibuni na juhudi za kidiplomasia za Iran zinazolenga kumaliza kabisa vita vinavyoendelea.
Araghchi alieleza wasiwasi wake kuhusu kile alichokitaja kuwa ni hatua za uchochezi za Marekani katika Ghuba ya Uajemi, pamoja na matamshi yasiyofaa kutoka kwa baadhi ya viongozi waandamizi wa Marekani. Alisema kuwa hatua hizo, sambamba na ukiukaji wa mara kwa mara wa usitishaji vita, zimeongeza mashaka kuhusu dhamira na uzito wa Marekani katika kufuata njia ya diplomasia.
Aidha, Waziri huyo alisema kuwa msimamo wa upande wa Marekani unaathiri vibaya mchakato wa diplomasia na unaongeza kutokuaminiana miongoni mwa wananchi wa Iran kuhusu nia halisi za Washington. Alisisitiza kuwa kusitishwa kwa mashambulizi yasiyo halali na kuachwa kwa misimamo ya kupindukia ni jambo la msingi katika kuendeleza mchakato wa sasa wa kidiplomasia.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, alisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa juhudi za kidiplomasia kwa lengo la kumaliza vita, na kueleza uungaji mkono wa Uturuki kwa mchakato wa sasa wa mazungumzo ya kidiplomasia.