Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, amelaani vikwazo vya Marekani dhidi yake kwa madai ya kuwaunga mkono waasi wa AFC/M23 mashariki mwa Kongo na kuvitaja kuwa “visivyo halali na vya matashi ya kisiasa.”
Ikitanza vikwazo hivyo siku ya Alhamisi, Idara ya Wizara ya Fedha ya Marekani Inayosimamia Udhibiti wa Mali za Kigeni ilimtuhumu Kabila kuwa amekuwa akilifadhili kifedha kundi la waasi wa AFC ili kuwa na ushawishi wa kisaisa mashariki mwa Kongo na kuwachochea wanajeshi wa kuachana na jeshi la taifa na kujiunga na safu ya waasi.
Ofisi ya Kabila imepinga na kupuuza vikwazo hivyo kwa sababu madai yaliyotolewa dhidi ya Joseph Kabila hayajathibitishwa hadi sasa.
Joseph Kabila alikuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, na anaishi Afrika Kusini tangu mwaka 2023.
Mapema mwaka jana, Kabila alijitokeza hadharani mashariki mwa Kongo katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi na kueleza nia yake ya kurejea nyumbani “kusaidia juhudi za kutafuta suluhisho” la mgogoro wa mashariki mwa Kongo.
Kabila amedai kuwa wakati wa uongozi wake alipata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na kuiunganisha nchi, kurejesha utulivu hatua kwa hatua na maridhiano ya kitaifa.