LONDON, Julai 13 – Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya usafiri wa baharini (IMO) limepinga mpango uliotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump wa kutoza ada ya asilimia 20 kwa mizigo yote inayosafirishwa kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz, likisema hatua hiyo haina msingi wa kisheria na inakiuka kanuni za kimataifa zinazolinda uhuru wa usafiri katika njia za kimataifa za baharini. Tamko hilo limetolewa kufuatia mpango wa Trump wa kurejesha ulinzi wa kijeshi wa Marekani katika eneo hilo na kuanzisha tozo hiyo kwa meli zinazopita katika njia hiyo muhimu ya biashara duniani.
Msemaji wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) alisema msimamo wa shirika hilo umebaki kuwa uleule kwamba hakuna taifa linaloruhusiwa kutoza ada kwa meli zinazopita katika njia za kimataifa za baharini kama Mlango wa Hormuz.
“Tunafahamu tangazo hilo na tunasubiri maelezo zaidi, lakini msimamo wetu ni kwamba kutoza ada kwa matumizi ya njia za kimataifa za baharini hakuruhusiwi chini ya sheria za kimataifa,” alisema msemaji wa IMO.
Awali, Trump alitangaza kupitia mtandao wake wa Truth Social kuwa Marekani itaanza tena kulinda Mlango wa Hormuz na kwamba asilimia 20 ya thamani ya mizigo yote itakayopita katika njia hiyo itatozwa kama malipo ya huduma za usalama. Hata hivyo, hakufafanua jinsi utaratibu huo utakavyotekelezwa wala msingi wake wa kisheria.
Tangazo hilo limeibua wasiwasi mkubwa kwa wadau wa sekta ya usafirishaji wa baharini na biashara ya kimataifa, wakieleza kuwa utekelezaji wa mpango huo unaweza kuongeza gharama za usafirishaji, kuathiri biashara ya kimataifa na kusababisha mabadiliko ya bei za mafuta, kwani takribani asilimia 20 ya mafuta yanayouzwa duniani hupitia Mlango wa Hormuz.
Kwa sasa, mataifa mbalimbali pamoja na wadau wa sekta ya usafiri wa baharini wanasubiri maelezo rasmi kuhusu namna mpango huo utakavyotekelezwa. Hata hivyo, msimamo wa Umoja wa Mataifa unaongeza shinikizo la kidiplomasia dhidi ya pendekezo hilo, huku ukisisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa zinazolinda uhuru wa usafiri katika njia za baharini zenye umuhimu mkubwa kwa uchumi wa dunia.
