TEHRAN, IRAN – Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amefichua mzozo mzito wa kidiplomasia uliopelekea upande wa Iran kusitisha ghafla mazungumzo na Marekani, kufuatia lugha ya vitisho kutoka kwa Rais wa nchi hiyo, Donald Trump.

Akielezea mkasa huo uliotokea katikati ya vikao vya majadiliano, Ghalibaf amesema kuwa alipata taarifa za kushtua kwamba Trump ametoa matamshi ya kibeberu yakilenga kumtishia Rais wa Iran, timu ya majadiliano, pamoja na vitisho vya kushambulia ardhi ya nchi hiyo.

Akizungumza kwa msimamo thabiti mbele ya mjumbe wa Marekani, naibu Rais, JD Vance, Spika Ghalibaf alimtaka mwanasiasa huyo kuelewa kuwa Iran haitayumbishwa.

Tuko hapa katika mazungumzo, na kwa mujibu wa makubaliano yaliyotiwa saini, kipengele cha kwanza kinakataza vitisho au shinikizo la aina yoyote. Hata hivyo, leo Rais wenu ametoa vitisho. Eleweni kuwa sisi hatujadiliani kamwe chini ya kivuli cha vitisho au shinikizo,” Ghalibaf alimweleza Vance kabla ya kuchukua uamuzi mgumu wa kusitisha mazungumzo hayo.

Inaarifwa kuwa mara baada ya kutoa kauli hiyo, ujumbe wa Iran uliondoka ukumbini na kukataa kurejea mezani, licha ya upande wa Marekani kujaribu kutafuta namna ya kuonana tena kupitia nchi wasuluhishi.

Licha ya jitihada za kidiplomasia zilizofanywa na wasuluhishi kutoka Qatar na Pakistan, Iran ilishikilia msimamo wake wa kutozungumza moja kwa moja na Marekani. Badala yake, Iran ilikubali kuwasiliana na wasuluhishi hao pekee ili kufikisha ujumbe wao.

Mvutano huo wa kidiplomasia uliodumu kwa dakika 80, uliazimia kutoa msimamo wa mwisho ambao baadaye uliwasilishwa kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na upande wa Qatar na Pakistan.

Tukio hili linaashiria msimamo mkali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kulinda heshima ya taifa hilo dhidi ya kile inachokiita kuwa ni sera za mabavu za mataifa ya Magharibi.

Leave a Reply