Waziri wakuu wa zamani wa Israel, Naftali Bennett na Yair Lapid, wametangaza kuunganisha rasmi vyama vyao na kuunda tiketi ya pamoja ya kisiasa itakayojulikana kama “Pamoja – Ikiongozwa na Naftali Bennett.”
Tangazo hilo lilitolewa Jumapili alasiri na msemaji wa Bennett. Akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa pwani wa Herzliya saa chache baadaye, Bennett alisema uamuzi wa kuungana na Lapid ni “hatua ya kizalendo na ya Kizayuni zaidi” ambayo wamewahi kuchukua kwa ajili ya maslahi ya nchi yao. Alisisitiza pia kuwa hatua hiyo inaashiria mwisho wa mgawanyiko wa kisiasa.
Bennett alieleza kuwa yeye na Lapid, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa upinzani, wanaendelea mbele kwa lengo la kupata ushindi katika uchaguzi ujao. Aidha, alimkaribisha mwenyekiti wa chama cha Yashar, Gadi Eisenkot, kujiunga na muungano huo, akisema kuwa mlango bado uko wazi kwa vyama na viongozi wengine wanaotaka kushirikiana.