Katibu mkuu wa Hezb Sheikh Naim Qassem2

Katibu Mkuu wa Hezb nchini Lebanon, Sheikh Naim Qassem, amesema kuwa usitishwaji wa mapigano nchini humo usingewezekana bila ushiriki wa Iran katika mazungumzo yaliyofanyika nchini Pakistan. Akizungumza kuhusu mchango wa Iran katika jitihada za amani, Sheikh Qassem alisema kuwa "kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isingekuwepo katika mazungumzo hayo, baada ya ushujaa na uvumilivu wa wananchi na wapiganaji wa Lebanon, kusingepatikana makubaliano ya kusitisha vita." Aliongeza kuwa serikali ya Lebanon haikupaswa kuchukua msimamo wa hasira dhidi ya hatua ya kusitisha vita, akisisitiza kwamba "hakuna mamlaka yoyote nje ya Lebanon yenye haki ya kuweka masharti kwa nchi hii." Kuhusu mashambulizi yaliyojulikana kama “Jumatano Nyeusi”, Sheikh Qassem alibainisha kuwa adui alifanya mashambulizi zaidi ya 200 ndani ya dakika 10 na kusababisha vifo vya mamia ya raia wasiokuwa na hatia, kisha kudai kuwa serikali ya Lebanon haina dhamira ya kusitisha mapigano. Aidha, alikosoa hatua ya serikali kukutana moja kwa moja na maofisa wa Marekani mjini Washington, akisema siku hiyo ilikuwa “ya fedheha kwa taifa.” Qassem alisema makubaliano yaliyopatikana yalikuwa ya upande mmoja, yakiiwezesha Israel kuendelea na mashambulizi yake huku yakilipachika kundi la wapiganaji wanaolinda Lebanon jina la “waasi”. Sheikh Qassem alihitimisha kwa kuuliza, “Je, serikali ya Lebanon inasimama upande wa adui?”