WASHINGTON/TEL AVIV –

Gazeti New York Times limeripoti kwamba Uhusiano wa kidiplomasia na kimkakati kati ya Marekani na Israel umechukua sura mpya, huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akionekana kuwekwa kando katika mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani na Iran.

Hapo awali, Rais Donald Trump alimchukulia Netanyahu kama mshirika wake mkuu na rubani mwenza katika harakati za kukabiliana na Iran. Hata hivyo, kufuatia kudorora kwa vita na kuanza kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano, Israel imejikuta ikitengwa kwa kiasi kikubwa katika majadiliano hayo.

Waziri Mkuu Netanyahu alikuwa na matumaini makubwa kuwa vita hivyo vingeangusha utawala wa Iran, kuharibu mpango wake wa nyuklia, na kutokomeza kabisa silaha zake za masafa marefu (makombora). Badala yake, hakuna hata kimojawapo kilichofanikiwa.

Rais Trump sasa ameelekeza nguvu zake katika kumaliza mzozo huo, hatua ambayo imeitenga Israel na kupunguza ushawishi wake kwenye makubaliano yoyote ya mwisho.

Kutokana na hali hiyo ya kutengwa, maafisa wa serikali ya Israel sasa wanalazimika kutegemea mawasiliano kutoka kwa washirika wao wa kikanda na taarifa za kijasusi ili kuweza kung’amua kile kinachojadiliwa kwa siri kati ya Washington na Tehran.

Kwa upande wa Netanyahu, athari za mabadiliko haya ni pigo kubwa kisiasa na kimkakati. Kiongozi huyo alijenga taswira yake ya kisiasa kwa kujinadi kuwa na ushawishi usio na kifani kwa Rais Trump. Lakini kwa hali ilivyo sasa, Israel inaonekana kutegemea kikamilifu idhini ya Marekani, hata katika kutekeleza maamuzi yake ya kijeshi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *