JOHANNESBURG, 17 Mei 2026 — Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema, amezua mjadala kufuatia kauli yake ya kuhoji namna janga la COVID‑19 lilivyodai maisha ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati John Magufuli, huku Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, akiendelea kuishi.
Akizungumza katika hafla ya kisiasa, Malema alimwelezea Magufuli kama “rais aliyekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa majukumu yake,” na kudai kuwa aliondolewa na virusi vya corona.
Katika maelezo yake, alihoji kwa nini janga hilo “halikumgusa” Mnangagwa, ambaye alimkosoa vikali kwa kumtaja kama kiongozi asiye na uwezo.
Kauli hiyo imeibua mjadala katika mitandao ya kijamii na miongoni mwa wachambuzi wa siasa, huku baadhi wakiona ni maoni ya kisiasa yenye lengo la kukosoa uongozi wa Zimbabwe, na wengine wakisisitiza umuhimu wa kuheshimu kumbukumbu za viongozi waliotangulia mbele ya haki.
Hadi sasa, hakujawa na majibu rasmi kutoka serikalini Zimbabwe kuhusu kauli hizo.