Mwandishi wa jarida la Kifaransa la Paris Match, Florian Tardif, ametoa madai mapya kuhusu kile alichodai kuwa ni chanzo cha mvutano kati ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mkewe Brigitte Macron.
Akizungumza na kituo cha redio cha RTL, Tardif — ambaye pia ni mwandishi wa kitabu “Wanandoa Wakamilifu” — alisema tukio lililosambazwa na Ikulu ya Élysée nchini Vietnam katika kipindi cha masika ya mwaka 2025 lilikuwa ni ugomvi kati ya rais huyo na mkewe.Kwa mujibu wa madai hayo, tofauti hiyo ilihusishwa na kile kilichoelezwa kuwa uhusiano wa “Kiplatoniki” kati ya Macron na mwigizaji wa Kiirani na Kifaransa, Golshifteh Farahani, mwenye umri wa miaka 42.
Tardif alidai hali hiyo ilipelekea Brigitte Macron kumpiga kofi mumewe.Hata hivyo, hadi sasa Ikulu ya Élysée pamoja na wahusika waliotajwa hawajathibitisha madai hayo.Wakati huo huo, gazeti la Le Figaro limechapisha taarifa hiyo kupitia majukwaa yake ya mtandaoni, huku mjadala mkubwa ukiendelea kusambaa katika mitandao ya kijamii nchini Ufaransa.