Mkuu wa tawi la Microsoft nchini Israel, Alon Haimovich, ameondoka rasmi kwenye wadhifa wake baada ya kuibuka kwa uchunguzi kuhusu matumizi ya teknolojia ya kampuni hiyo na vyombo vya ulinzi vya Israel katika shughuli za upelelezi dhidi ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa gazeti la kifedha la Globes, Haimovich amejiuzulu baada ya kuhudumu kwa miaka minne kama meneja mkuu wa Microsoft Israel. Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa usimamizi wa shughuli za kampuni hiyo nchini Israel sasa utahamishiwa chini ya Microsoft France.
Hatua hiyo inafuatia uchunguzi ulioanzishwa na Microsoft mwaka uliopita kuhusu matumizi ya jukwaa lake la huduma za kompyuta ya wingu, Azure, na jeshi la Israel.
Mfumo huo unadaiwa kutumiwa kuendesha mtandao wa ufuatiliaji uliokuwa na uwezo wa kurekodi, kurudia na kuchambua maudhui ya mamilioni ya simu za Wapalestina kila siku.
Uchunguzi huo ulianzishwa baada ya taarifa kufichua kuwa kitengo cha ujasusi cha Israel kinachojulikana kama Unit 8200 kilitumia Azure kuhifadhi kiwango kikubwa cha mawasiliano yaliyodukuliwa kutoka Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Wakati huo huo, mameneja kadhaa wa idara ya utawala ndani ya Microsoft Israel nao wameondoka kwenye nyadhifa zao kutokana na hofu ya uwezekano wa ukiukwaji wa maadili na sera za kampuni hiyo.
Microsoft bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu matokeo ya uchunguzi huo wala sababu kamili za kuondoka kwa viongozi hao.