Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametembelea kambi ya timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Iran kabla ya kuondoka kuelekea Kombe la Dunia, akiwahimiza wachezaji na benchi la ufundi kujituma kikamilifu ili kuiletea nchi heshima.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Jumatano kwenye kituo cha mazoezi cha timu ya taifa, rais huyo alikutana na wachezaji, makocha pamoja na viongozi wa shirikisho la mpira wa miguu la Iran. Katika mazungumzo yake, alisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano wa kitaifa, pamoja na kuonyesha hadhi na nguvu ya watu wa Iran katika jukwaa la kimataifa kupitia michezo.
Akilihutubia kikosi hicho, Pezeshkian alisema jambo muhimu ni juhudi za dhati, uwajibikaji na kutumia uwezo wote uliopo kwa ajili ya kuleta fahari kwa taifa. Aliongeza kuwa wananchi wa Iran wanatarajia wachezaji wao kusimama kwa heshima na kupambana kwa nguvu zote wanapokuwa uwanjani.
Rais huyo pia alieleza kuwa michezo, hususan mpira wa miguu, ina nafasi muhimu katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kuongeza mtaji wa kijamii na kuleta fahari miongoni mwa wananchi.
Katika hafla hiyo, Pezeshkian alikabidhiwa jezi namba 12 ya timu ya taifa ya Iran, ambayo kwa kawaida huwakilisha mashabiki wa timu hiyo.