Iran imedai kuwa majeshi ya Marekani yamekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano baada ya kushambulia tanker ya mafuta ya Iran iliyokuwa ikielekea Mlango wa Hormuz kutoka maji ya pwani karibu na Jask.

Kulingana na taarifa hiyo, shambulio hilo pia lilihusisha chombo kingine kilichokuwa kinaingia katika njia ya maji mkabala na Bandari ya Fujairah katika Falme za Kiarabu (UAE), pamoja na maeneo ya kiraia.

Kwa mujibu wa jeshi la Iran, vikosi vyake vilijibu mara moja kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi, yakilenga mali za kijeshi za Marekani mashariki mwa Mlango wa Hormuz.

Vyanzo vya Iran vimeripoti kuwa baadhi ya vitengo vya majini vya Marekani vilipata uharibifu, huku meli za kivita za Marekani zikionekana kuondoka katika eneo hilo.

Hata hivyo, Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imesema majeshi yake yalichukua hatua za kujilinda baada ya kudai kuzuia makombora ya Iran, ndege zisizo na rubani na boti ndogo.

Kwa mujibu wa Marekani, hakuna mali zake za kijeshi zilizoharibiwa na mashambulizi hayo yalilenga miundombinu ya kijeshi ya Iran pekee.Iran kwa upande wake imesisitiza kuwa makabiliano hayo yalianza kutokana na kile ilichokiita uchokozi wa Marekani, ikionya kwamba mashambulizi yoyote zaidi yatakabiliwa na majibu ya haraka na makali.

Tukio hilo limeongeza wasiwasi wa kuongezeka kwa mvutano katika Mlango wa Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafiri wa baharini duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *