Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametoa onyo kali dhidi ya kile alichokiita ongezeko la chuki dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ndani ya Marekani, akidai kuwa mwelekeo huo ni tishio kwa mataifa yote mawili.
Akizungumza jana Jumapili katika mahojiano na kipindi cha The Sunday Briefing cha Fox News, Netanyahu alijibu kauli za Makamu wa Rais, JD Vance, huku akikemea makundi ya kisiasa yanayopinga Israel. Netanyahu ameeleza wasiwasi wake juu ya mrengo wa “Woke Right” na baadhi ya wanachama wa Chama cha Democratic, akidai kuwa mipasuko hiyo inahatarisha ushirika wa kihistoria uliopo.
Katika kuelezea uzito wa jambo hilo, Netanyahu alisema:
“Ninatiwa wasiwasi na kuwepo kwa mwelekeo huu unaoipinga Israel… Nitafanya kila niwezalo kurekebisha hali hii. Kumbukeni, wale wanaochukia Israel, hatimaye huanza kuichukia Marekani pia.”
Hatua hii ya Netanyahu inatafsiriwa kama mkakati wa kidiplomasia wa kujaribu kuunganisha msaada wa kisiasa nchini Marekani wakati ambapo upinzani dhidi ya sera za Israel ukiendelea kushika kasi duniani. Wachambuzi wanaona kuwa kauli hizi zinaweza kuzidisha mjadala wa ndani ya vyama vya siasa nchini Marekani kuhusu kiwango cha msaada wa kijeshi na kidiplomasia kwa taifa hilo.