Mtu mmoja amepoteza maisha na wengine wanne kujeruhiwa vibaya kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya mabomu yaliyolenga makazi ya wanasiasa watatu wa chama tawala cha New Democracy katika mji wa Thessaloniki, kaskazini mwa Ugiriki.

Jeshi la polisi nchini humo limethibitisha kuwa washambuliaji hao walitumia mabomu ya kienyeji kutekeleza ukatili huo. Mashambulizi hayo yaliyofanyika kwa uratibu wa karibu, yalitokea kwa kufuatana ndani ya muda wa dakika 15 tu nyakati za alfajiri.

Wanasiasa waliolengwa katika mashambulizi hayo ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho, Zisis Ioakimovich, Mbunge wa zamani Savvas Anastasiadis, pamoja na aliyekuwa mgombea wa chama hicho, Aphrodite Nestora.

Duru za kitabibu kutoka hospitali ya Thessaloniki zimeeleza kuwa, mama mzazi wa mwanasiasa Aphrodite Nestora amefariki dunia akiwa hospitalini kutokana na majeraha makali aliyoyapata. Mumewe (baba mzazi wa mwanasiasa huyo) pia amelazwa hospitalini hapo akipatiwa matibabu kufuatia majeraha aliyopata kwenye shambulio hilo.

Hadi sasa, polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini waliohusika na mtandao huo wa kigaidi.

Leave a Reply