Shirika la Habari la Fars, likinukuu chanzo cha uhakika, limeripoti kuwa hakutakuwa na mazungumzo yoyote kati ya Iran na Marekani bila kufanyika kwa uhamishaji wa fedha za Iran zilizozuiwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mzozo mkubwa wa hivi punde kati ya mataifa haya mawili kuelekea kuanza kwa mazungumzo, unahusu utaratibu wa kuiwezesha Iran kufikia mali zake hizo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, suala la fedha za Iran zinazoshikiliwa linashughulikiwa kupitia juhudi za upatanishi zinazoongozwa na nchi ya Qatar. Imeelezwa pia kuwa hapo awali, Marekani ilikiuka ahadi zake kuhusiana na urejeshwaji wa mali hizo za Iran.
Chanzo hicho kimeiambia Fars kuwa Iran imeshikilia msimamo wake thabiti, ikisisitiza kwamba maadamu fedha hizo zilizokubaliwa hazijahamishwa, hakuna makubaliano yoyote yanayoweza kufikiwa baina yao.
Hata hivyo, mashauriano yanayoendelea nchini Qatar yameripotiwa kupiga hatua nzuri kuelekea kutatua kikwazo hicho.
Licha ya hatua hiyo, chanzo hicho kimebainisha kuwa jopo la wapatanishi la Iran halichukulii maelewano hayo ya awali kama uamuzi wa mwisho, hasa kutokana na rekodi ya Marekani ya kukiuka makubaliano huko nyuma. Kimeongeza kuwa Iran imethibitisha kuwa iko tayari kwa hatua na chaguzi zote zinazoweza kujitokeza.