Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, ametangaza wazi kuwa azma ya nchi yake kujiunga na Umoja wa Ulaya (EU) si kipaumbele kikuu cha sera za kigeni za Ankara kwa sasa, akionya kuwa iwapo nchi za Ulaya zitaendelea kuifungia milango Uturuki, wao ndio watakaobeba mzigo mkubwa wa hasara za kijiopolitiki na kiusalama.
Katika mahojiano maalum na mtandao wa habari wa Al Jazeera, Erdoğan alieleza kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya hazijaonyesha nia ya dhati au utayari wa kuijumuisha Uturuki ndani ya umoja huo, licha ya miongo kadhaa ya mazungumzo na mikataba ya ushirikiano. Rais huyo alisisitiza kuwa Uturuki imejenga mwelekeo huru wa kiuchumi, kijeshi, na kidiplomasia unaoiwezesha kutegemea washirika mbalimbali duniani bila kutegemea uamuzi wa Brussels.
Mchakato wa Uturuki kuomba uanachama wa EU ulianza rasmi mwishoni mwa miaka ya 1980 na mazungumzo rasmi ya kujiunga yalianza mwaka 2005. Hata hivyo, mazungumzo hayo yamekuwa katika mkwamo wa muda mrefu kutokana na tofauti za kisiasa, migogoro ya kijiografia (hususan suala la Cyprus), na mivutano ya kisheria na kiutawala kati ya pande hizo mbili.