IRAN imesisitiza kuwa haitafanya makubaliano yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama wa taifa, uhuru na mipaka yake, huku ikiendelea kusisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kidiplomasia katika kumaliza mvutano wa kijeshi ulioanzishwa na Marekani na Israel.
Naibu Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Bagheri Kani, ametoa msimamo huo Jumatatu, Novemba 2, wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, mjini Beijing.
Bagheri Kani amesema Tehran haitalegeza msimamo wake kuhusu kulinda mamlaka na maslahi ya taifa, licha ya shinikizo na vitisho vya kijeshi vinavyoendelea kutoka Washington.
Amesema mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yameonesha hatari ya kutumia nguvu za kijeshi kutatua migogoro ya kimataifa, akionya kuwa kuendeleza vita kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa dunia.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao pia wamejadili juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita na kuimarisha usalama wa kudumu katika Mashariki ya Kati.
Kwa upande wake, Wang Yi amesema China inaunga mkono haki ya Iran ya kulinda uhuru, usalama na mamlaka yake ya kitaifa.
Waziri huyo amesisitiza kuwa migogoro ya Mashariki ya Kati inapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo ya kisiasa badala ya kuendeleza matumizi ya nguvu.
Msimamo huo unakuja wakati Marekani ikiendelea kutoa vitisho vya kuanzisha tena operesheni za kijeshi dhidi ya Iran, huku Tehran ikionya kuwa shambulizi lolote jipya litakabiliwa na jibu kali la kijeshi.

Maoni