Meli ya kivita ya Marekani ikiwa baharini wakati wa operesheni za kijeshi Mashariki ya Kati

WASHINGTON / TEHRAN — Uwepo mkubwa wa kijeshi wa Marekani katika Mashariki ya Kati unakabiliwa na mkwamo mkubwa wa kiugavi kufuatia hatua ya Iran kulemaza miundombinu tegemezi ya Jeshi la Majini la Marekani katika ukanda wa Ghuba.

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la The New York Times, operesheni za Marekani zinazohusisha meli za kivita 20 na takriban askari na mabaharia 20,000 zimekuwa ngumu mno kujiendesha. Kikosi hicho kinahitaji zaidi ya galoni milioni 8 za mafuta na milo 420,000 kila wiki.

Kufuatia mashambulizi ya Iran yaliyoharibu kituo kikuu cha ugavi cha Marekani nchini Bahrain, pamoja na vitisho vya droni na makombora kwenye bandari nyingine za kikanda, jeshi hilo limepoteza mtandao wake wa karibu wa huduma. Meli za ugavi sasa zinalazimika kusafiri umbali wa maili 2,200 kuelekea kisiwa cha Diego Garcia, au hadi maili 3,700 kuelekea Singapore, ili kuchukua vifaa na kurejea Bahari ya Kiarabu na Ghuba ya Oman.

Mkuu wa Jeshi la Majini la Marekani, Admirali Daryl Caudle, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo, akieleza kuwa wanajeshi “hawatarudi Bahrain hivi karibuni” kutokana na kuharibika kwa miundombinu na kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji.

Hali hii inatajwa na wachambuzi wa masuala ya ulinzi kama ushindi wa kimkakati wa Tehran unaotumia mbinu za “kuzuia ufikiaji wa eneo” (A2/AD), unaolilazimisha jeshi kubwa zaidi duniani kutumia rasilimali na muda mwingi kujiendesha kuliko kufanya operesheni za ulinzi.

Leave a Reply